Saturday, 15 August 2009

KUIGA TUNAKOIGA, TWAIGA NA VYA KIJINGA?


Vipo vingi vya kuiga, vinavyopaswa kuigwa,


Hivyo mtu akiiga, hata yeye ataigwa,


Ubaya siyo kuiga, ni vile vinavyoigwa,


Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?





Mashindano ya urembo, tumeiga asilani,


Wanatao kwa mapambo, wandele majukwaani,


Wanasa kama urimbo, na nusu nguo mwilini,


Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?





Hilo tumelikubali, tukasema ni modeni,


Vichupi na suluali, na mavazi ya fukweni,


Wakiyajibu maswali, kwa lafudhi za kigeni,


Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?





Twashindanisha watoto, kwenye urembo jamani,


Urembo huo ni ndoto, kwa watoto wa shuleni,


Watoto wawe watoto, twadhulumu jamani,


Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?





Hebu pita kijiweni, mwangalie Solomoni,


Suruali matakoni, na kofia kisogoni,


Aimba Kimarekani, kakulia Kiwalani,


Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?





Tunaporudi nyumbani, twatoka ughaibuni,


Twajifanya ni wageni, tumesahau kingoni,


Ndoo ya maji bafuni, twataka ya mvua jamani,


Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?





Tuige vilivyo bora, vyenye tunu na thamani,


Tusiwe tunajichora, kwa kuiga vya kihuni,


Tuige bila papara, vya kutupa ahueni,


Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?




1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

Kaka.
Kazi njema saana mkuu. Nashukuru kwa shairi hili ambalo linazungumzia mengi ya kweli kutuhusu. Sina a kuongeza hapa zaidi ya kukumbusha niliyogusia kuhusiana na maisha yetu ambayo waweza kujikumbusha kupitia link hii (http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/03/kizazi-kipya-kizazi-kinachorithishwa.html) na pia katika hii pia (http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/03/tunazidi-kujipoteza-katika-harakati-za.html)
Heshima na Amani kwako Kaka
Blessings