Monday, 13 July 2009

Ndege asiyewindwa akinasa aliwe?




Wa kijiji nimetinga, na swali nawapangia,

Magwiji toka Iringa, wa Tanga naulizia,

Na wa pwani mnotunga, fanya hima kujibia,

Ndege asiyewindwa, akinasa aliwe?



Ametoka bwana Kombo, keenda zake kuwinda,

Mtego kaweka chambo, ni kwale anawawinda,

Kashinda huko kitambo, huku roho yamdunda,

Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?



Mtego ukafyatuka, sauti ikasikika,

Ndipo Kombo akaruka, na kisu akakishika,

Mtegoni akazuka, kuona kilonasika,

Ndege asiyewindwa, akinaswwa aliwe?



Kunasa kanasa Kanga, kwale amenusurika,

Kwale kaula mpunga, kisha akapeperuka,

Makosa kafanya kanga, mtegoni kashikika,

Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?



Ndipo Kombo kaudhika, aliyemtaka karuka,

Jambo Kanga analika, ngoma iko kupikika,

Kwale alitamanika, mtegoni kaponeka,

Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?



Ndipo saa nauliza, Kisu kimlambe kanga?

Nini kitamtuliza, mtani kutoka Tanga,

Kombo anajiuliza, amuachilie Kanga?

Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?



Kaditamati natama, natama nikatuwama,

Nilichotaka kusema, kukisema nimesema,

Kompyuta ninazima, kwenye fikara nazama,

Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?



Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji).



No comments: